Saturday, 3 June 2017

WAZIRI DKT. TIZEBA: “WEZESHENI WASINDIKAJI MAZIWA ILI KUONGEZA TIJA TASNIA YA MAZIWA”


Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba (kushoto), akizungumza na maofisa wa Benki ya Kilimo juu ya umuhimu wa kuharakisha utoaji wa mikopo kwa wasindikaji wa maziwa nchini. (Na Mpiga Picha Wetu).

Na Mwandishi Wetu, Bukoba
Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles Tizeba ameiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) kuharakisha kutoa mikopo kwa wasindikaji wa maziwa nchi ili kuongeza tija kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini.
Waziri Dkt. Tizeba alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa Benki hiyo katika Kilele cha Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki ya Maziwa iliyokuwa ikifanyika Kitaifa mjini Bukoba, mkoani Kagera tangu tarehe 28 Mei na kufikia kilele chake tarehe 01 Juni, 2017.

Dkt. Tizeba alisema utoaji wa mikopo kwa wasindikaji una umuhimu wa kipekee kwa kuwa utachangia uhakika wa masoko kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini hali itakayochochea tija kwa wafugaji hao hivyo kuchagiza lengo la Serikali la Awamu ya Tano ya kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuweza kunufaika na sekta hizo.

“Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi hivyo uanzishwaji wa Benki ya Kilimo lazima usaidie katika kuhakikisha wasindikaji wa maziwa wanapata huduma za TADB kwa wakati ili tupate uhakika wa masoko kwa wafugaji wetu ili tuiinue Tasnia ya Maziwa ili ichangie ukuaji wa uchumi na maendeleo nchini,” alisema.

Kwa mujibu wa mpango kazi wa TADB, sekta ya mifugo ni mojawapo ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa nchini. Na Benki imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa Ufugaji wa Ng’ombe wa Nyama na Maziwa ili kuongeza tija kwenye Tasnia za nyama na maziwa ili kuchagiza maendeleo katika tasnia hizo.
Katika kuhakikisha wasindikaji wa maziwa wananufaika na huduma za TADB, Benki hiyo inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).

Kwa mujibu wa Mpango Kazi huo, mikopo hiyo ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

TADB ni taasisi ya serikali ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini ambao ulikuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi; masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

KIKOSI CHA TAIFA STARS CHAENDELEA KUJIFUA HUKO ALEXANDRIA, MISRI


Wachezaji wa Taifa Stars wakipasha joto miili yao kabla ya kuanza mazoezi ya nguvu kwenye Uwanja wa Tolip Sports City jijini Alexandria leo asubuhi Juni 01, 2017. Taifa Stars inajiandaa kushindana na Lesotho Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.

Makipa wa Taifa Stars kutoka kushoto, Said Mohammed, Aishi Manula na Benno Kakolanya wakivuta pumzi baada ya mazoezi ya timu ya Tanzania ya Mpira wa Miguu ‘Taifa Stars’ yaliyofanyika jana usiku kwenye Uwanja wa Tolip Sports City jijini Alexandria jana usiku Mei 31, 2017. Taifa Stars inajiandaa kushindana na Lesotho Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.

Daktari wa Viungo wa Taifa Stars, Dk. Gilbert Kigadye akimfanyisha mazoezi ya kifundo cha mguu beki wa timu hiyo, Mohammed Hussein Zimbwe maarufu kama Tshabalala katika mazoezi ya timu ya Tanzania ya Mpira wa Miguu ‘Taifa Stars’ yaliyofanyika Uwanja wa Tolip Sports City jijini Alexandria jana usiku Mei 31, 2017.

Wachezaji wa Stars wakiwania mpira katika mazoezi ya nguvu yaliyofanyika leo. Taifa Stars inajiandaa kushindana na Lesotho Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.
Wachezaji wa Stars kutoka kushoto, Mohammed Hussein, Simon Msuva, Said Mohammed, Ibrahim Ajib na Hassan Kessy wakionyesha faraja yao mara baada mazoezi ya nguvu yaliyofanyika leo. Taifa Stars inajiandaa kushindana na Lesotho Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.






MALINZI: TANZANIA IPO TAYARI KWA AFCON U-17

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi amesema Tanzania imejiandaa vema kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya vijana waliochini ya miaka 17 za Afrika zitakazofanyika nchini 2019.
Akizungumza na wandishi wa habari jana Malinzi alisema Tanzania imeanza maandalizi kujenga timu imara ambayo italeta ushindani kwani Serengeti boys imeonyesha njia.
“Timu itakayoshiriki Afcon U-17 mwaka 2019 ilianza kuandaliwa tangu 2013 kwa mashindano ya U-14 yaliyofanyika Mwanza na sasa wapo kambini Mwanza na TFF inawagharamia kila kitu,” alisema Malinzi.
Pia Malinzi alisema ili nchi iwe mwenyeji wa mashindano ya vijana unatakiwa kuwa na viwanja viwili jambo ambalo Tanzania inakidhi hadi hoteli na barabara zinazounganisha hoteli watakazofikia timu na kwenda uwanjani
“Mei 28 Rais wa CAF ndugu Ahmad alimkabidhi Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa uenyeji wa fainali za U-17 za mwaka 2019 tukio ambalo lilishuhudiwa na dunia nzima,” alisema Malinzi.
Aidha Malinzi alisema ni aibu nchi kuwa mwenyeji halafu timu ikaondolewa katika hatua ya makundi hivyo benchi la ufundi lina kazi ya kuandaa timu imara ndio maana wamelazimika kuwaamisha wachezaji kutoka Mwanza na kuwaleta Dar es Salaam.
Alisema Kamati ya maandalizi ya CAF itakuja nchini kuangalia maandalizi ya viwanja vya mashindano na mazoezi, hoteli na barabara zitakazotumika wakati timu zikienda uwanjani.
Katika kuthibitisha Tanzania imejiandaa kufanya maandalizi ya kutosha Malinzi alisema watamtumia Rais wa zamani wa TFF, Leodgar Tenga ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya maandalizi wa fainali za wanawake za Afrika zilizopita awape uzoefu wa vitu vinavyoangaliwa.
Alisema Tanzania inaweza kupata nafasi ya kucheza kombe la Dunia zijazo kwani FIFA imeongeza wigo kwa nchi za Afrika kuwa tisa hadi 10 ikiwa ni uwiano wa timu moja katika kila timu tano za Afrika kwani Afrika zipo 55.